Samson Kakwila vs Semeni Shedrack (Rufaa No. 2038 of 2026) [2026] TZHC 3037 (10 Juni 2026)
Judgment
MAHAKAMA YA TANZANIA MAHAKAMA KUU YA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA MASJALA NDOGO KIGOMA INAYOKETI KIGOMA RUFAA NO. 000002038 OF 2026 SAMSON KAKWILA .............................. MLALAMIKAJI/ MRUFANI/ MWOMBAJI/ MDAI DHIDI YA SEMENI SHEDRACK .............................. MJIBU MAOMBI/ MRUFANIWA/ MDAIWA HUKUMU RWIZILE, J 20 Mei na 10 June 2026 Katika rufaa hii mrufani anapinga uamuzi wa Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya ya Kasulu, wa kuondoa Maombi ya Ardhi Na. 03 ya Mwaka 2023 kwa kigezo cha kutounganishwa kwa wadaawa muhimu kwenye maombi hayo. Uamuzi huo, ulifanywa na Baraza hilo tarehe 18 Desemba 2025 baadaya kupokea ushahidi wa pande zote. Inaonekana katika kumbukumbu za maombi hayo, mrufni alifungua maombi akidai eneo lake kuvamiwa na mjibu rufaa kwa ukubwa wa hatua 4 kwa 12.5 Kurasa. 1
lenye thamani ya TZS 1,000,00.00, enao lililopo katika kijiji cha Nyachenda, Wilaya ya Kasulu. Baada ya kusikiliza mashidi wa pande zote, Baraza katika uamuzi wake, liliona shauri halikustahili kuwepo mbele yake kwa sababu mrufani hakuunganisha wadaawa muhimu. Hivyo katika Uamuzi wake, Mwenyekiti wa Baraza alitoa somo la nani hasa ni mdaawa muhimu. Mwisho maombi hayo yalifukuzwa. Hata hivyo, mrufani hakuridhika na umuzi huo, akata rufaa kwa sababu zifuatazo;
- Kwamba, Mheshimiwa Mwenyekiti alikosea sana kisheria na kimantiki kwa kuamua kiini kilichohusiana na kutowaunganisha wadaawa muhimu ambao ni Siajali Samson Kakwila na Medas Sadock Lumoli kwa kuliondosha Barazani Shauri la Maombi ya Ardhi Na. 03 la Mwaka 2023 bila kuwapa fursa wadaawa wa shauri hilo kutoa hoja zao kuhusiana na kiini hicho.
- Kwamba, Kwa nguvu ya ushahidi kama ulivyotolewa na Mrufani kwenye kumbukumbu, Mheshimiwa Mwenyekiti alikosea kisheria na kimantiki alipoamua kuwa Siajali Samson Kakwila na Medas Sadock Lumoli walipaswa kuunganishwa kwenye shauri hilo la Maombi ya Ardhi Na. 03 la Mwaka 2023 kama wadaawa muhimu. Kwa upande wake, Mjibu rufaa aliomba mahakama itupilie mbali rufaa hii kwani Baraza lilifikia uamuzi sahihi wa kuyaondoa maombi ya Mrufani kwa kushindwa kukidhi kigezo muhimu cha kuwaunganisha wadaawa muhimu katika shauri hilo. Mrufani aliwakilishwa na wakili msomi Bwana Method RG Kurasa. 2
Kabuguzi, Mjibu rufaa alisimama mwenyewe, bila uwakilishi Akiwasilisha hoja za Mrufani, wakili Kabuguzi alieleza katika sababu ya kwanza ya rufaa kwamba, mara baada ya kusikilizwa kikamilifu kwa Maombi ya Ardhi Na. 03 ya Mwaka 2023, Mwenyekiti wa Baraza alifikia umauzi uliotokana na hoja aliyoibua kwa utashi wake binafsi huku akiwanyima wadaawa haki ya kusikilizwa kuhusu hoja ya kutounganishwa kwa wadaawa muhimu katika maombi hayo. Alisema, hii haikuwa sahihi, maana hata hao aliodai walipaswa kuungnishwa walikuwa sehemu ya mashahidi wa mrufani. Katika sababu ya pili, wakili Kabuguzi alieleza kwamba hapakuwa na haja ya kuwaunganisha watu hao waliotajwa kama wadaawa muhimu katika shauri hilo kwani ushahidi uliokuwepo ulijitosheleza, Baraza lingeweza kufanya maamuzi. Hivyo, aliomba Mahakama kufuta uamuzi wa Baraza na kulielekeza kutoa uamuzi wa maombi kwa kuzingatia ushahidi uliopo mbele yake. Mjibu rufaa kwa upande wake, alisema hakujua nini kilitokea katika Baraza. Alisema kwamba, wakati Siyajali ananunua eneo la mgogoro yeye alikuwa ni shahidi wake, lakini baadae naye alilinunua eneo hilo na kuna mashahidi walioshuhudia na wala hapakuwahi kutokea mgogoro wa mipaka ya eneo hilo. Amehitimisha kwa kueleza kwamba ushahidi ulijitosheleza kwani hukumu ingeweza kutolewa na Baraza kwa kuzingatia ushahidi wa pande zote. Hoja yake hii, hata hivyo ni tofauti na majibu yake ya sababu za rufaa. Baada ya kupitia kwa umakini kumbukumbu za Baraza hususani mwenendo wa shauri husika na uamuzi, ni ukweli usiopingika kwamba baada ya Kurasa. 3
kusikiliza ushahidi wa pande zote, Mwenyekiti alibaki na jukumu moja tu la kuandaa na kutoa hukumu. Hata hivyo, katika hukumu yake, Mwenyekiti wa Baraza aliibua hoja ngeni ya kisheria ambayo imepelekea kupingwa kwa hukumu hiyo na Mrufani. Hoja hiyo ni kutounganishwa kwa wadaawa muhimu ambao ni wanunuzi/wauzaji wa ardhi ya mgogoro kabla ya Mjibu rufaa kuinunua. Kimsingi, malalamiko ya Mrufani ni kutokupewa fursa ya kusikilizwa baada ya Baraza kuibua hoja hiyo. Kitu ambacho mjibu rufaa hapingani nacho. Pia, Mrufani anaamini kwamba pasipo haja ya kujikita katika hoja hiyo, ushahidi uliopo mbele ya Baraza hilo unajitosheleza kutolewa uamuzi bila kujali uwepo au kutokuwepo kwa watu ambao Baraza limeona kama ni wadaawa muhimu waliostahili kuwa sehemu ya maombi hayo ya ardhi. Hoja hii pia mjibu rufaa, hapingani nayo katika wasilisho lake fupi. Ni utaratibu wa kisheria, pale ambapo mahakama inaibua hoja kwa utashi wake yenyewe, hutakiwa kutoa fursa ya kusikilizwa pande husika katika shauri hilo kabla ya kufikia maamuzi kutokana na hoja hiyo. Kinyume na hivyo maamuzi yanayotolewa bila kuwapa fursa ya kusikilizwa, yanakiuka haki ya msingi ya kusikilizwa. Kwa kuwa usikilizwaji wa maombi ulikuwa umeshafungwa, Baraza kwa kuona umuhimu wa hoja mpya iliyoibuliwa, lilipaswa kuwaita tena wadaawa, na kuwapa fursa kutoa maoni yao kuhusu hoja hiyo. Haikuwa sahihi kwa mtazamo wangu, kuanza kutoa somo la nani hasa ni mdaawa muhimu katika shauri bila kuwashirikisha wadaawa. Baraza lilikuwa na wajibu kuzisikiliza Kurasa. 4
pande zote mbili kabla ya kuamua kutoa hukumu yake. Mahakama ya Rufani kwenye shauri la Jayantkumar Chandubhai Patel @ Jeetu Patel & Others vs The Attorney General & Others (Civil Application No.160 of 2016) [2019] TZCA 571 (28 May 2019) katika ukurasa wa 31, iliseama kama ifuatavyo; “…it is our firm finding that the judgment under review was arrived at without affording the parties an opportunity to be heard on the new matter raised by the Court suo motu. What the Court ought to have done upon uncovering the new matter was to re-open the hearing and require the learned counsel for the parties to address it on the issue…” Kwa tasfiri “…ni msimamo wetu thabiti kwamba hukumu inayorejewa ilifikiwa bila kuzipa pande zote fursa ya kusikilizwa kuhusu jambo jipya lililoibuliwa na Mahakama yenyewe (suo motu). Kile ambacho Mahakama ilipaswa kufanya baada ya kugundua jambo hilo jipya, ilikuwa ni kufungua tena usikilizaji na kuwataka mawakili wasomi wa pande zote mbili kutoa hoja zao kuhusu suala hilo…” Kwa mukatadha huo, ni dhahiri Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya lilikosea kutowapatia fursa ya kusikilizwa pale lilipoibua hoja juu kutounganishwa kwa wadaawa muhimu katika maombi hayo. Hivyo sababu ya kwanza ya rufaa inamashiko. Katika sababu ya pili ya rufaa, ni makubaliano ya pande zote mbili kwamba ushahidi uliotolewa ulitosheleza, Baraza kutoa hukumu. Ni dhahiri kusema Kurasa. 5
kuwa katika maelezo ya mashahidi hakuna sehemu inonyesha wahusika muhimu hawakuwepo kiasi cha kufikiri kukosekana kwao kungeathiri hukumu na tuzo. Hivyo ninakubaliana pia na sababu ya pili ya rufaa. Baada ya kupitia sababu zote za rufaa, nakubaliana na mapendekezo ya wakili wa Mrufani kwamba uamuzi wa Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya Kasulu wa kufuta maombi ya mrufani kwa kigezo kilichotajwa hapo juu unapaswa kutenguliwa kwa makosa ya kisheria yaliyobainishwa hapo juu. Kwa maana hiyo, chini ya kifungu cha 47 cha Sheria ya Mahakama za Migogoro ya Ardhi [Sura ya 216 Rekebu la 2023] uamuzi huo wa Baraza unatenguliwa. Shauri hilo linarejeshwa katika Baraza hilo kwa ajili ya kutoa uamuzi kutokana na ushahidi uliopo kwenye kumbukumbu na mwenendo wa Baraza hilo. Nadhani ni muhimu pia kwa mazingira ya shauri hili kuelekeza kila upande kujilipia gharama zake. Imetolewa katika AKAMA KUU YA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA MASJALA NDOGO KIGOMA INAYOKETI KIGOMA tarehe 10 Juni 2026. A. K RWIZILE Kurasa. 6
JAJI Kurasa. 7