Anasia Sindakila Tinya vs Tito Lazaro Sindakila and Others (RUFAA YA MIRATHI NO. 2280 OF 2026) [2026] TZHC 3057 (5 June 2026)
Judgment
MAHAKAMA YA TANZANIA MAHAKAMA KUU YA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA MASJALA NDOGO KIGOMA INAYOKETI KIGOMA RUFAA YA MIRATHI NO. 000002280 OF 2026 ANASIA SINDAKILA TINYA .............................. MLALAMIKAJI/ MRUFANI/ MWOMBAJI/ MDAI DHIDI YA TITO LAZARO SINDAKILA .............................. MJIBU MAOMBI/ MRUFANIWA/ MDAIWA JACKSON JAPHET FUMBO .............................. MJIBU MAOMBI/ MRUFANIWA/ MDAIWA EMANUEL LAZARO SINDAKILA .............................. MJIBU MAOMBI/ MRUFANIWA/ MDAIWA HUKUMU RWIZILE, J Katika rufaa hii, mrufani anapinga hukumu ya Mahakama ya Wilaya ya Buhigwe katika Rufaa Namba 29767 ya mwaka 2025. Katika rufaa hiyo, Mahakama ilikubaliana na uamuzi ya Mahakama ya Mwanzo Manyovu katika shauri la Mirathi Namba 11 ya mwaka 2025. Mrufani, kwa mujibu wa kumbukumbu za shauri hilo, aliomba kuteuliwa kuwa msimamizi wa mirathi Kurasa. 1
ya Marehemu Sindakila Tinya. Hata hivyo Mjibu rufaa Na, 1, aliweka pingamizi akiomba, pamoja na mambo mengine, Mahakama isikubali ombi lake kwa kuwa hakuteuliwa na kikao cha familia. Mahakama ilikubaliana na pingamizi hilo na kufukuza maombi yake. Kwa kuwa hakuridhika na uamuzi huo wa mahakama ya wilaya, Mrufani amekuja tena mbele ya mahakama, akijaribu kupinga hukumu hiyo kwa sababu zifuatazo;
-
Kwamba Mahakama ya Wilaya Buhigwe ilikosea kisheria na kimantiki ilipothibitisha maamuzi ya Mahakama ya mwanzo Manyovu kwa mapingamizi yaliyoibuliwa na wajibu rufaa wakati hawana mamlaka juu ya mirathi ya marehemu LAZARO SINDAKILA na mirathi ya bibi yao. Hivyo maamuzi yaliyofikiwa kuwa batili.
-
Kwamba, Mahakama ya Wilaya Buhigwe ilikosea kisheria na kimantiki ilipothibitisha maamuzi ya mahakama ya mwanzo Manyovu ilipojielekeza vibaya kuwa mirathi ya marehemu inasimamiwa na sheria ya mirathi wakati kuna mgogoro wa ardhi ambapo ilishindwa kuzingatia umiliki wa ardhi hivyo mgogoro ulisikilizwa kabla ya wakati wake.
-
Kwamba, Mahakama ya Wilaya ya Buhigwe ilikosea kisheria na kimantiki ilipothibitisha maamuzi ya Mahakama ya Mwanzo Manyovu kwa kujielekeza kwenye ushahidi wa kujichanganya wa Wajibu rufaa kuhusiana na kikao cha familia pamoja na mirathi ya marehemu SINDAKILA TINYA wakati madai hayo sio sababu tosha za Muomba rufaa kutoteuliwa kuwa msimamizi wa mirathi. Kurasa. 2
-
Kwamba, Mahakama ya Wilaya ya Buhigwe ilikosea kisheria na kimantiki ilipothibitisha maamuzi ya Mahakama ya Mwanzo Manyovu ilipopuuzia kuwa hakuna ushahidi ulitolewa kuthibitisha usimamizi wa mirathi marehemu ya marehemu SINDAKILA na mke wake kwani imeshagawiwa au kuteuliwa kuwa msimamizi wa mirathi, hivyo mahakama ilikosea kuthibitisha maamuzi ya mahakama ya mwanzo Manyovu.
-
Kwamba, mahakama ya Wilaya Buhigwe ilikosea kisheria na kimantiki ilipothibitisha maamuzi ya mahakama ya Mwanzo Manyovu kwa kuhitimisha kuwa marehemu SINDAKILA TINYA hakuacha mirathi ambayo inaweza kusimamiwa bila kuzingatia kuwa ushahidi wa Mjibu rufaa EMANUEL LAZARO SINDAKILA kuwa kuna mali baadhi hazikutajwa, hivyo mahakama ya wilaya ilifikia maamuzi bila kuchambua ushahidi.
-
Kwamba, Mahakama ya Wilaya ya Buhigwe ilikosea kisheria na kimantiki ilipothibitisha maamuzi ya Mahakama ya Mwanzo Manyovu kwa madai kuwa kikao cha wanafamilia ni takwa la kisheria wakati sio kweli.
-
Kwamba, Mahakama ya Wilaya ya Buhigwe ilikosea kisheria na kimantiki ilipothibitisha maamuzi ya Mahakama ya Mwanzo Manyovu kwa kushindwa kuchambua ushahidi wa Muomba rufaa na mashahidi wake hivyo kufikia maamuzi batili. Rufaa hii, ilisikilizwa kwa njia ya maandishi. Mrufani alipata huduma ya Wakili Msomi Bw. Silvester Damas Sogomba. Hata hivyo, wajibu rufaa kwa pamoja waliandaa wenyewe wasilisho lao. Hawakuwa na uwakilishi. Baada ya Kurasa. 3
kupokea mawasilisho yao na kupitia kumbukumbu za shauri katika Mahakama ya Mwanzo, Mahakama ilibaini suala la kisheria ambalo lilipelekea iwaalike pande zote kulizungumzia kabla ya kulitolea uamuzi. Hii ni kwa sababu mwenendo wa shauri katika Mahakama ya Mwanzo ulikiuka taratibu na jambo hili halikuwa sehemu ya sababu za rufaa. Hivyo waliombwa kutoa ufafanuzi; Kama taratibu za usikilizwaji wa pingamizi dhidi ya Mrufani kuteuliwa kusimamia mirathi ya marehemu Sindakila Tinya zilifuata kianuni ya 5 ya Kanuni za Mahakama za Mwanzo (Usimamizi wa Mirathi) (Marekebisho) ya Mwaka 2025, Tangazo la Serikali Na. 428 la tarehe 11/07/2025, na mahakama ya Mwanzo. Katika kujibu hoja hiyo Wakili Sogomba alisema japo kwa ufupi kwamba taratibu hizikufuatwa kwani Mahakama ilisikiliza pingamizi dhidi ya mrufani. Kwa sababu hiyo, alipendekeza Mahakama kufutilia mbali mwenendo wa shauri katika Mahakama ya Mwanzo na kulirejesha mbele yake ili utaratibu wa kisheria ufuatwe. Kwa upande wao wajibu rufaa, kupitia kwa mjibu rufaa wa 2, wameeleza kutokufahamu kilichotokea. Hata hivyo, wameiomba mahakama ifanye masahihisho kwenye kasoro iliyoibuliwa. Ikumbukwe katika Mahakama za Mwanzo mashauri ya mirathi yanaongozwa na Kanuni katika Jedwali la 5 la Sheria ya Mahakama za Mahakimu [Sura ya 11 Rekebu ya 2023]. Kanuni hizo zimefanyiwa marekebisho na Kanuni za Mahakama za Mwanzo (Usimamizi wa Mirathi) (Marekebisho) ya Mwaka 2025 Tangazo la Serikali Na. 428 la tarehe 11/07/2025. Kurasa. 4
Pamoja na masuala mengineyo, Kanuni hizo zimeeleza utaratibu wa kushughulika na pingamizi dhidi ya mtu anayeomba kuteuliwa kuwa msimamizi wa mirathi katika Mahakama ya Mwanzo. Kwa rejea, Kanuni ya 5(6) ya Kanuni hizo inaelekeza; “Pale ambapo pingamizi limewekwa na mtu yeyote mwenye maslahi, mahakama itaandika/itanukuu pingamizi hilo, itamtaka mwombaji kuthibitisha maombi yake, itasikiliza pingamizi na kuamua iwapo ikubali au ikatae maombi hayo.” Kumbukumbu za Mahakama ya Mwanzo husani mwenendo wa shauri wa tarehe 06/10/2025 kuanzia ukurasa wa 3 zinaonyesha kuwa baada ya kupokea pingamizi la Tito Lazaro Sindakila akipinga uteuzi wa mrufani kuwa msimamizi wa mirathi, Mahakama ilijielekeza moja kwa moja katika usikilizwaji wa pingamizi hilo, kwa kuita mashahidi wa mpingaji kwanza. Mara baada ya kusikiliza upande wa mpingaji Mahakama ilisikiliza majibu ya pingamizi kutoka kwa mrufani,amabaye naye aliita mashahid wake. Kisha Mahakama kutoa uamuzi wa kukubaliana na pingamizi hilo, ikisema mrufani, hastahili kuteuliwa kuwa msimamizi wa mirathi ya Marehemu Sindakila Tinya. Hii ni kinyume kabisa na Kanuni na taratibu za usikilizwaji wa Mirathi kwani kanuni imelekeza anasikilizwa kwanza mleta maombi. Kwa kawaida, Mahakama inapopokea pingamizi, ambayo kwa kawaidi linaweza kuletwa katika hatua yoyote, kabla ya mirathi kufungwa. Katika hatua za awali, kama ilivyokuwa katika shauri hili. Pingamizi kwa usahihi lililetwa kabla ya kuteule Kurasa. 5
msimamizi wa mirathi. Likipinga uteuzi wake ambayo ni hatua ya kawaida kufanya hivyo. Mahakama kwa hiyo, ilipaswa kuchukua hatua zifuatazo; a. Kumwita mwombaji na kumtaarifu kuhusu pingamizi husika kama ambavyo ilifanya. b. Kuwataarifa hatua inayofuata ya namna ya kusikiliza shauri husika. Ni utaratibu wa uliozoeleka na kukubalika, kwamba Mahakama ikipokea pingamizi katika hauta kama hiyo, ina takiwa kwanza kumsikiliza mwombaji. Katika kufanya hivyo, maombi yanageuka na kuwa kama shauri la madai la kawaida na hivyo kufuata misingi ya kisheria ya usikilizwaji was mashauri ya madai, angalia shauri la Monica Nyamakare Jigamba dhidi Mugeta Bwire Bhakome as an administrator of the estate of Musiba Reni Jigabha and Another (Civil application No. 199 of 2019) [2020] TZCA 1820 (16 October 2020). Hivyo, si tu kwa mujibu wa kanuni 5(6) niliyoinukuu hapo juu, mahakama ilitakiwa kufuata maelekezo ya Mahakama za juu. Msingi wake, ni kuanza kusikiliza mleta maombi amabaye anachukuliwa kama mdai, na akisha maliza kutoa ushahidi wake, vielelezo kama anavyo na kuita mashahid kama wapo, mleta pingamizi atasikilzwa kama vile mdaiwa kwa kufuata taratibu za kawaida za uendeshaji mashauri ya madai. Ni katika muktadha huo pingamizi lake litasikilzwa na uamuzi wa ama kumteua au kukubali pingamizi litaamriwa. Kurasa. 6
Kama nilivyoonyesha hatua hii haikufikiwa na hivyo mrufani aliyepeleka maombi yake hayakusikilizwa, bali alijibu tu pingamizi kinyume na utaratibu. Hivyo, ni wazi pingamizi dhidi ya uteuzi wake lilisikilizwa na kutolewa uamuzi kinyume na utaratibu wa kisheria. Mrufani alipendekeza mwenendo wa shauri la Mahakama ya Mwanzo ufutwe, shauri lirejeshwe katika Mahakama ya Mwanzo ili usikilizwaji ukafanyike kwa mujibu wa sheria. Nakubaliana na mapendekezo hayo. Njia pekee ya kurekebisha mapungufu hayo, ni kufuta hukumu na amri za Mahakama ya Wilaya na pia hukumu na Mwenendo wa Mahakama ya Mwanzo . Hivyo basi, kupitia kifungu cha 30(2) cha Sheria ya Mahakama za Mahakimu [Sura ya 11 Rekebu la 2023] ninalazimika kufuta mwenendo was shauri katika Mahakama ya Mwanzo Manyovu kuanzia pale ambapo Mahakama ilianza kusikiliza pingamizi la Tito Lazaro Sindakila. Sambamba na hilo, shauri hili linarejeshwa katika Mahakama hiyo ili kuanza kusikilizwa kwa mujibu wa sheria zilizotajwa hapo juu kuanzia pale ambapo pingamizi lilipokelewa. Katika kutekeleza matakwa ya kanuni hiyo, shauri lisikilizwe na Hakimu mwingine mwenye mamlaka. Kila upande utabeba gharama zake. Imetolewa katika AKAMA KUU YA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA MASJALA NDOGO KIGOMA INAYOKETI KIGOMA tarehe 5 Juni 2026. Kurasa. 7
A. K RWIZILE JAJI Kurasa. 8