africa.lawBeta
SearchAsk AICollectionsJudgesCompareMemo
africa.law

Free access to African legal information. Legislation, case law, and regulatory documents from across the continent.

Resources

  • Legislation
  • Gazettes
  • Jurisdictions

Developers

  • API Documentation
  • Bulk Downloads
  • Data Sources
  • GitHub

Company

  • About
  • Contact
  • Terms of Use
  • Privacy Policy

Jurisdictions

  • All jurisdictions →

© 2026 africa.law by Bhala. Open legal information for Africa.

Aggregating legal information from official government publications and public legal databases across the continent.

Back to search
Case Law[2026] TZHC 2842Tanzania

Jumanne Rashidi Nkwanyi (Administrator of the Estate of the Late Rashidi Nkwanyi) vs Saidi Idd Hussein (Land Appeal No. 266 OF 2026) [2026] TZHC 2842 (2 June 2026)

High Court of Tanzania

Judgment

MAHAKAMA YA TANZANIA MAHAKAMA KUU YA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA MASJALA NDOGO KIGOMA INAYOKETI KIGOMA RUFAA NO. 000000266 OF 2026 JUMANNE RASHIDI NKWANYI (ADMINISTRATOR OF THE ESTATE OF THE LATE RASHIDI NKWANYI) .............................. MLALAMIKAJI/ MRUFANI/ MWOMBAJI/ MDAI DHIDI YA SAIDI IDD HUSSEIN .............................. MJIBU MAOMBI/ MRUFANIWA/ MDAIWA HUKUMU RWIZILE, J 22 Aprili na 2 Juni 2026. Hii ni rufaa kutoka Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya Kigoma katika maombi Na. 22 ya mwaka 2023. Maomba Mbele ya Baraza yalifunguliwa na mjibu rufaa. Baada ya Baraza hilo kusikiliza ushahidi na hoja za pande zote mbili, lilitoa hukumu yake tarehe 28 Novemba 2025 na kumtambua Mjibu Rufaa kuwa mmiliki halali wa eneo la ardhi lenye mgogoro, lenye ukubwa wa hatua ishirini (20) na upana wa hatua mbili (2).Aidha, Baraza liliamuru Mrufani kuondoa jengo au maendeleo yoyote aliyoyafanya katika eneo hilo la Kurasa. 1

mgogoro na kulipa gharama za shauri. Mrufani hakuridhishwa na hukumu hiyo, kisha kuleta rufaa katika Mahakama haya akipinga uamuzi wa Baraza kwa sababu tisa (9) , kama zinavyoainishwa hapa chini:-

  1. Kwamba, kutokana na ushahidi dhaifu uliowasilishwa na Mjibu rufaa ambaye ndiye aliyekuwa muombaji, Baraza la ardhi na nyumba wilaya ya Kigoma lilikosea kisheria na kimantiki kuamua kuwa Mjibu rufaa alikuwa amethibitisha madai yake kama yalivyorekebishwa katika viwango vinavyotakiwa kisheria.
  2. Kwamba, Baraza la ardhi wilaya lilikosea kisheria kumpa ushindi Mjibu rufaa juu ya eneo lenye mgogoro alilolitambulisha kama uchochoro wa hatua 20 urefu kwa upana hatua mbili ( 20x2) pasipo uthibitisho wa umiliki na ukubwa wa eneo lake kwa upande mmoja na mipaka ya kipande anachodai kwa upande mwingine kutoka eneo la Mwomba rufaa.
  3. Kwamba, Baraza la ardhi na nyumba wilaya ya Kigoma lilikosea kisheria na kimantiki lilipompa Mjibu rufaa, nafuu zinazokinzana na maombi aliyoyasilisha barazani pamoja na ushahidi wake.
  4. Kwamba, kwa vile baraza lilipokea vielelezo vya Mwomba rufaa kumiliki ekari moja ambamo ndani yake Mjibu rufaa aliwahi kuvamia na kujenga choo na kisha kukiri uvamizi huo mwezi May, 2016 na kuondolewa ( kielelezo B3), na baadaye mwaka 2023 akadai eneo hilohilo kama uchochoro, basi baraza la ardhi wilaya lilikosea kisheria na kimantiki kuamini kuwa Mjibu rufaa alikuw? amevamiwa na Mwomba rufaa ambaye yumo na kajenga ndani ya mipaka ya Kurasa. 2

shamba lake. 5. Kwamba, katika mazingira ya mgogoro huu unaohusu mpaka mdogo sana kati ya wadaawa (uchochoro), baraza lilikosea kisheria na kimantiki kutokutembelea eneo gombaniwa licha ya kuombwa kufanya hivyo na wadaawa na hivyo kutoa hukumu juu ya mipaka pasipo uhakika nayo. 6. Kwamba, kwa vile Mjibu rufaa alikiri katika kuhojiwa kuwa eneo lake lilikwisha wekewa alama ya X yaani kuondoka kwa kuwa limo ndani ya hifadhi ya barabara, basi Baraza la ardhi lilikosea kimantiki kuamini kuwa Mjibu rufaa alibaki na eneo analolidai isipokuwa mbinu ya kujitanua baada ya kuuziwa hifadhi ya barabara na shahidi wake pekee SM2 (Subi Ismail). 7. Kwamba, baraza lilikosea kisheria na kimantiki kupokea na kusikiliza madai ya Mjibu rufaa kuhusu uchochoro ulioko kijijini ambao kimsingi ni njia ya umma isiyomilikiwa na mtu yeyote kama mali binafsi, pasipo kusikiliza au kujumuishwa kwa serikali ya kijiji/kitongoji cha Machazo 'A' inayosimamia njia za umma kijijini na hivyo kuvunjwa kwa misingi ya usikilizwaji na ujumuishwaji wa wadaawa muhimu. 8. Kwamba, baraza la ardhi na nyumba la wilaya ya Kigoma lilikosea kisheria kutopokea baadhi ya vielelezo vya Mwomba rufaa ikiwa ni pamoja na ramani ya eneo lenye mgogoro iliyochorwa na Mahakama ya mwanzo Ujiji katika Shauri la mirathi Na.43 ya 2009 pasipo sababu za msingi kisheria na hivyo kufifisha nguvu ya utetezi wa mwomba rufaa. Kurasa. 3

  1. Kwamba, Mhe. Mwenyekiti wa baraza alikosea kisheria kukubaliana na maoni ya wajumbe/washauri wa baraza ambao kimsingi walibadili jukumu la kuthibitisha madai kutoka kwa Mjibu rufaa kama mwombaji kuwa la mwomba rufaa hii kama mjibu maombi. Rufaa hii ilisikilizwa kwa njia ya maandishi; Mrufani aliwasilisha hoja zake kwa kupitia Wakili Ignatius R. Kagashe, Mjibu Rufaa naye akiwasilisha hoja zake kwa kupitia Wakili Daniel Rumenyera. Katika wasilisho lake kwa niaba ya mrufani, Wakili Kagashe aliondoa sababu ya tisa ya rufaa, lakini aliunganisha sababu ya kwanza, ya pili, ya nne, ya sita na ya saba za rufaa na kuzitolea maelezo ya pamoja. Akieleza kwamba mrufani alishindwa kuthibitisha kuwa eneo la mgogoro lina urefu wa hatua ishirini (20) na upana wa hatua mbili hadi tatu (2–3). Wakili alirejea uamuzi katika shauri la Martin Fredrick Rajab dhidi ya Ilemela Municipal Council & Synergy Tanzania Company Limited [2022] TZCA 434 (TANZLII), ambapo Mahakama ya Rufani ilisisitiza, mdai anapaswa kubainisha kwa uwazi ukubwa, mipaka na alama za eneo analolidai. Wakili Kagashe aliendelea kueleza kuwa, ingawa Mjibu Rufaa alidai kuwa alinunua ardhi hiyo kutoka kwa Subi Ismail mwaka 1993, hakuwasilisha mkataba wa mauziano wala ushahidi mwingine unaobainisha mipaka ya eneo husika. Aidha, shahidi wake, Subi Ismail, alieleza tu kuwa maeneo hayo yalitenganishwa na njia ya kwenda mtoni, maelezo ambayo, kwa mujibu wa Kurasa. 4

Mrufani, hayakutosha kubainisha eneo hilo kisheria. Wakili aliendelea kueleza kwamba kwa upande wake, Mrufani aliwasilisha mkataba wa mauziano wa ekari moja uliopokelewa kama kielelezo B2 pamoja na barua ya kuomba radhi ya Mjibu Rufaa iliyopokelewa kama kielelezo B3 kufuatia madai ya uvamizi wa eneo hilo mwaka 2016. Hata hivyo, alidai kuwa Baraza halikufanya tathmini ya kina ya ushahidi huo. Vilevile, wakili alieleza kwamba Baraza halikuthamini ipasavyo ushahidi wa shahidi wa utetezi DW2 ambaye alithibitisha kuwa ardhi hiyo iligawiwa kwa Mrufani mwaka 1989. Katika kuimarisha hoja hiyo, alirejea shauri la Sangijo Rice Millers Company Limited dhidi ya East African Development Bank [2006] TLR 91 na Selemani Mtumba dhidi ya Juma Bwenge, Rufaa ya Madai Na. 115 ya 2015. Aidha, Wakili Kagashe aliwasilisha kuwa Baraza lilibadili wajibu wa uthibitisho kinyume na masharti ya vifungu vya 110, 111 na 112 vya Sheria ya Ushahidi, Sura ya 6 [Rekebu la mwaka 2023]. Katika kuunga mkono hoja hiyo, alirejea uamuzi katika shauri la Jonas Jonas dhidi ya The Registered Trustees of the Roman Catholic Church of Musoma Diocese, Rufaa ya Madai Na. 33 ya 2016. Wakili Kagashe aliendelea kueleza kuwa, ingawa Baraza lilinukuu uamuzi wa Godfrey Sayi dhidi ya Anna Siame , akiwa Mwakilishi Mary Mndolwa, kuhusu kanuni ya wajibu wa uthibitisho, alisema, lilikosea katika matumizi Kurasa. 5

yake kwa kuwa, kwa maoni yake, hakukuwa na ushahidi wa kutosha kuthibitisha madai ya uvamizi wa eneo lenye urefu wa futi ishirini (20) na upana wa futi mbili (2). Alirejea maamuzi ya Standard Chartered Bank Tanzania Limited dhidi ya National Oil Tanzania Limited na Mwenzake. Kuhusu sababu ya tano ya rufaa, Wakili aliwasilisha kwamba Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya lilikosea kisheria na kimantiki kwa kushindwa kutembelea eneo la mgogoro (locus in quo) licha ya maombi yaliyotolewa na wahusika. Alirejea uamuzi wa shauri la Registered Trustees of Telesina Sisters na Wenzake 10 dhidi ya Nassoro Thamit Lipangile (Msimamizi wa mirathi ya marehemu Rukia Lipangile) na Mwenzake [2024] TZCA 1241, ambapo Mahakama ya Rufani ilieleza kuwa ukaguzi wa eneo la mgogoro ni muhimu kwa ajili ya kusaidia Mahakama au Baraza kubaini ukweli wa mambo yanayobishaniwa. Wakili alieleza kwamba kushindwa kutembelea eneo la mgogoro kuliliweka Baraza katika mazingira ya kufikia hitimisho bila kuwa na taswira kamili ya eneo husika na mazingira yake. Katika sababu ya nane ya rufaa, Wakili Kagashe alilalamikia uamuzi wa Baraza kwa kukataa kupokea baadhi ya vielelezo alivyodai vilikuwa muhimu katika kuamua mgogoro huo. Alivitaja vielelezo hivyo kuwa ni pamoja mchoro (sketch map) iliyochorwa katika Shauri la Mirathi Na. 43 la mwaka 2009 pamoja na nyaraka nyingine ambazo, kwa mujibu wake, zingeweza kusaidia kubainisha mipaka ya eneo la mgogoro na historia ya umiliki wa ardhi husika. Kurasa. 6

Kwa ujumla, mrufani aliiomba Mahakama kuikubali rufaa hii, kutengua hukumu na amri za Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya ya Kigoma zilizotolewa katika Shauri la Ardhi Na. 22 la Mwaka 2023, na kuamuru shauri lisikilizwe upya mbele ya Baraza lenye mamlaka. Au kwa njia mbadala, Mahakama iamuru Baraza husika kutembelea eneo la mgogoro (locus in quo) kabla ya kutoa uamuzi. Aidha, aliomba Mrufani apewe gharama zake. Kwa upande wa Mjibu rufaa alieleza kuwa alikuwa ametoa ushahidi thabiti na wa kutosha uliokiwezesha baraza la ardhi la wilaya kutoa hukumu sahihi. Ili kuthibitisha ushindi huo, alimleta shahidi aliyeitwa Subi Ismail, ambaye pande zote mbili zinasadiki kuwa ndiye aliyewauzia ardhi hiyo yeye pamoja na marehemu Rashid Nkwanyi. Ushahidi wa Subi Ismail unapatikana kwenye ukurasa wa 36 wa kumbukumbu za shauri katika baraza hilo za tarehe 01/07/2025. Kuhusu maelezo ya mipaka ya ardhi hiyo, mjibu rufaa alibainisha kuwa yalifafanuliwa vyema na yeye mwenyewe (kama shahidi wa kwanza) pamoja na Subi Ismail. Aliongeza kuwa mrufani hakuwahi kudai kwamba hajui eneo hilo, na hivyo madai yoyote mapya ni yakufikirika ( afterthought ). Hii, inasabishwa na kupuuzwa kwa uamuzi katika shauri la Abbas Anthony Kilumile dhidi ya Deremsi Msena ulizingatiwa. Mjibu rufaa alifafanua kuwa mrufani, akiwa kama msimamizi wa mirathi ya marehemu Rashidi Nkwanyi, hakuwa na mamlaka ya kujenga ukuta kwenye Kurasa. 7

ardhi hiyo kwa kuwa kuendeleza ardhi si jukumu la msimamizi wa mirathi. Alirejea uamuzi wa Mahakama Kuu ya Tanzania (Moshi) katika shauri la Sekunde Mbwambo dhidi ya Rose Ramadhani [2004] TLR 439, ikisisitiza kuwa jukumu la msimamizi ni kukusanya mali na kuzigawa kwa warithi stahiki, na si kuzidhibiti au kuanza kujenga kabla ya kuziwasilisha kwa warithi. Mjibu rufaa alibainisha kuwa mrufani aliwasilisha mkataba wa mauzo (kielelezo B2) kati ya marehemu na Subi Ismail ambao haukuonyesha mipaka ya ekari hiyo moja, jambo linalofanya mkataba huo kukosa thamani ya kiushahidi. Aliiomba mahakama tukufu kufanya tathmini upya ya ushahidi ili kuthibitisha kuwa mrufani aliingia kwenye ardhi yake bila ruhusa ( trespass ) na kusababisha nyumba yake kupasuka. Kuhusu hoja ya kwamba baraza halikutembelea eneo la mgogoro ( locus in quo ), mjibu rufaa alieleza kuwa hakuna upande wowote ulioomba utaratibu huo ufanyike. Hatimaye, alihitimisha kuwa kielelezo kilichotajwa kwenye hoja ya nane hakikuwasilishwa kwa sababu halali, mchora ramani hiyo hakuwa anajulikana, huku akipinga madai kuwa ilichorwa na Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo ya Ujiji kwa kuwa mahakama haina mamlaka ya kuchora ramani Kurasa. 8

Baada ya kupitia kwa makini mawasiliho ya pande zote, kupitia mwenendo mzima wa shauri pamoja na hukumu ya Baraza; hoja ya msingi inayopaswa kuamriwa na Mahakama ni iwapo rufaa hii inamashiko kisheria. Hata hivyo, nitaanza kushughulika na sababu ya rufaa ya tano inayohusu kushindwa kutembelea eneo la mgogoro. Kutokana na kumbukumbu za shauri, mgogoro uliokuwa mbele ya Baraza ulihusu mpaka kati ya wadaawa, hususani eneo lililoelezwa kuwa ni uchochoro wenye urefu wa hatua ishirini (20) na upana wa hatua mbili hadi tatu (2–3). Mjibu Rufaa alidai kuwa Mrufani alivamia sehemu ya eneo hilo kwa kujenga msingi wa jengo, wakati kwa upande wake Mrufani alikanusha madai hayo na kudai kuwa ni Mjibu Rufaa ndiye aliyevamia eneo lake kwa kuchimba shimo la choo. Kutokana na asili ya mgogoro huo ambao ulihusisha madai yanayokinzana kuhusu eneo halisi la mpaka na matumizi ya eneo la mgogoro, ushahidi wa kuona hali halisi ya eneo husika ungekuwa na umuhimu mkubwa katika kubaini ukweli wa madai ya kila upande. Katika mazingira hayo, kutembelea eneo la mgogoro kungeliwezesha Baraza kupata taswira halisi ya eneo linalobishaniwa, mipaka yake, pamoja na maendeleo yaliyodaiwa kufanywa na kila upande. Kwa hiyo, suala linalohitaji kuchunguzwa na Mahakama ni iwapo Baraza kutotembelea eneo la mgogoro kulisababisha dosari katika uchunguzi wa ukweli wa mgogoro huo na hivyo kuathiri usahihi wa hitimisho katika uamuzi Kurasa. 9

uliofikiwa. Ni kweli kwamba kutembelea eneo la mgogoro si takwa la lazima la kisheria katika kila shauri. Mamlaka ya kufanya ukaguzi wa eneo la mgogoro yapo ndani ya busara ya Mahakama au Baraza husika, na hutumika pale ambapo mazingira ya shauri yanaonesha kuwa hatua hiyo ni muhimu ili kuthibitisha, kufafanua au kuondoa shaka kuhusu ushahidi uliotolewa na pande zinazohusika. Katika shauri la Dar es Salaam Water na Sewerage Authority dhidi ya Didas Kameka na Wenzake, Rufaa ya Madai Na. 233 of 2019 [2021] TZCA 596 (18 October 2021), Mahakama ya Rufani ieleza kama ifuatavyo: "We are mindful of the fact that there is no law which forcefully and mandatorily requires the court or tribunal to inspect a locus in quo, as the same is done at the discretion of the court or tribunal, particularly when it is necessary to verify evidence adduced by the parties during trial." Kwa tafsiri "Tunatambua kuwa hakuna sheria inayolazimisha Mahakama au Baraza kutembelea eneo la mgogoro (locus in quo), kwani kufanya hivyo ni hiari ya Mahakama au Baraza, hasa kunapokuwepo umuhimu wa kuthibitisha ushahidi uliotolewa na pande husika wakati wa usikilizwaji wa shauri." Kurasa. 10

Kutokana na kumbukumbu za shauri hili, kila upande uliwasilisha madai yanayokinzana kuhusu eneo linalodaiwa kuvamiwa. Mjibu Rufaa alidai kuwa Mrufani alivamia sehemu ya eneo la mgogoro kwa kujenga msingi wa nyumba, ilihali Mrufani alidai kuwa ni Mjibu Rufaa ndiye aliyevamia eneo lake ambalo aliacha kama uchochoro kwa kujenga shimo la choo. Eneo linalobishaniwa lilielezwa kuwa na urefu wa hatua ishirini (20) na upana wa hatua mbili hadi tatu (2–3). Kwa maoni ya Mahakama, mazingira ya mgogoro huu, mipaka na matumizi ya eneo linalobishaniwa ndiyo hoja ya msingi, jambo ambalo lingeweza kubainishwa kwa urahisi zaidi kupitia ukaguzi wa eneo la mgogoro. Pia shauri la Registered Trustees of Telesina Sisters na wenzake kumi(10) dhidi ya Nassoro Thabit Lipangile (Msimamizi wa mirathi ya marehemu Rukia Lipangile) na Mwenzake, Rufaa ya Madai Na. 382 ya 2021 [2024] TZCA 1241, ambapo Mahakama ilisema: "As to whether visiting locus in quo was necessary in this case, we have judged that it was. The nature of the dispute as reflected in the record of appeal justifies visiting locus in quo. It appears that parties were not in common understanding as to the identity of the disputed land or at least the location, description and boundaries were in dispute between the parties." Kwa tafsiri Kurasa. 11

" Kuhusu suala la iwapo ilikuwa ni lazima kufanya ukaguzi wa eneo la mgogoro katika shauri hili, tumebaini kwamba ilikuwa ni muhimu kufanya hivyo. Asili ya mgogoro kama inavyoonekana katika kumbukumbu za rufani inaonesha umuhimu wa ukaguzi huo. Inaonekana kuwa wahusika hawakuwa na uelewano kuhusu utambulisho wa ardhi inayogombaniwa au angalau kulikuwa na mgogoro kuhusu mahali ilipo, maelezo yake na mipaka yake." Kadhalika, katika shauri la Victor Raphael Luvena dhidi ya Magreth Ephraim Kawa na Wenzake, Rufaa ya Madai Na 25 ya 2021,Mahakama ilieleza kwamba: "The main purpose of visiting the locus in quo is to verify facts and claims that cannot be conclusively established through oral testimony or documentary evidence presented before the court or tribunal." Kwa tafsiri "Lengo kuu la kutembelea eneo la mgogoro ni kuthibitisha ukweli wa mambo na madai ambayo hayawezi kubainishwa kikamilifu kupitia ushahidi wa mdomo au nyaraka zilizowasilishwa mbele ya Mahakama au Baraza." Kwa kuzingatia kanuni hizo za kisheria na mazingira ya shauri hili, Mahakama inaona kwamba mgogoro uliokuwa mbele ya Baraza ulihusu Kurasa. 12

eneo linalodaiwa kuvamiwa, mahali lilipo, mipaka yake na maendeleo yaliyofanywa na kila upande. Haya ni masuala ambayo yasingeweza, kwa maoni yangu, kubainishwa kwa uhakika kwa kutegemea ushahidi wa mdomo pekee. Katika mazingira hayo, Mahakama inaona kuwa Baraza lingefanya haki zaidi kwa kutembelea eneo la mgogoro ili kujiridhisha kuhusu ukweli wa madai yaliyotolewa na pande zote mbili kabla ya kufikia hitimisho lake. Aidha, Mahakama imepitia kwa makini mwenendo mzima wa shauri pamoja na hukumu ya Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya. Kutokana na kumbukumbu za shauri, imebainika kuwa tarehe 13/05/2023, Baraza lilitoa amri ya kutembelea eneo la mgogoro. Hata hivyo, siku hiyo Wakili wa Mjibu Maombi alieleza kuwa ukaguzi huo usingeweza kufanyika kwa kuwa Wakili wa Mwombaji hakuwepo mahakamani. Vilevile, aliomba pingamizi lililokuwepo lisikilizwe na kuamriwa kwanza kabla ya hatua ya ukaguzi wa eneo la mgogoro kufanyika. Baada ya hatua hiyo, Mahakama haijaona sehemu yoyote katika kumbukumbu za rufaa zinazoonesha kuwa Baraza liliendelea kutekeleza amri yake ya awali kwa kutembelea eneo la mgogoro. Wala hakuna kumbukumbu inayoonesha kuwa amri hiyo ilifutwa au kubadilishwa. Kwa hiyo, ni dhahiri kwamba ukaguzi wa eneo la mgogoro ambao hapo awali ulionekana kuwa muhimu na Baraza lenyewe haukufanyika. Kurasa. 13

Mahakama inaona kasoro hiyo ya kutotembelea eneo la mgogoro ni ya msingi. Ni ya msingi, kwa sababu mgogoro uliokuwa mbele ya Baraza ulihusu mpaka wa ardhi kati ya pande zote, ambapo kila upande uliutuhumu upande mwingine kuvamia eneo analodai kuwa lake. Eneo lenyewe lilielezwa kuwa ni sehemu ya eneo lenye takribani hatua ishirini (20) kwa urefu na hatua mbili hadi tatu (2–3) kwa upana. Katika mazingira hayo, ukaguzi wa eneo la mgogoro ungelipatia fursa Baraza kuona hali halisi ya eneo husika, mipaka yake, alama za kudumu zilizopo, maendeleo yaliyofanywa na kila upande, pamoja na uhusiano wa maeneo yanayodaiwa na wahusika. Kutokufanyika hivyo kumesababisha Baraza kutegemea maelezo yanayokinzana ya mashahidi bila kuwa na ushahidi ambao ungeweza kusaidia kufafanua ukweli wa mgogoro uliokuwa mbele yake. Matokeo yake ni kwamba Baraza lilifikia hitimisho kuhusu mgogoro wa mpaka wa ardhi bila kuwa na msingi wa kutosha wa ukweli wa mambo uliotokana na uchunguzi wa eneo husika. Hali hiyo iliathiri usahihi wa hukumu yake na hatimaye kuathiri haki kwa pande zote mbili. Kwa mantiki hiyo, Mahakama inakubaliana na sababu ya tano ya rufaa na kuiona kuwa ina mashiko. Kwa kuwa sababu ya tano ya rufaa inatosha kuamua rufani hii, sioni ulazima wa kujadili sababu nyingine za rufaa yaani sababu ya 1, 2,3,4,6, 7 na 8 . Kurasa. 14

Mahakama inakubaliana na rufani hii. Hukumu na amri za Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya ya Kigoma katika Shauri la Ardhi Na. 22 la Mwaka 2023 zinatenguliwa. Kumbukumbu za shauri zinarejeshwa kwenye Baraza hilo kwa maelekezo kwamba litembelee na kuchunguza eneo la mgogoro kwa kuzingatia taratibu zote za kisheria na kutoa hukumu kwa kuzingatia matokeo ya ukaguzi huo pamoja na ushahidi wote uliopo kwenye kumbukumbu za shauri. Ili kuondoa shaka, Baraza linapaswa kuongozwa na mwongozo uliowekwa na Mahakama ya Rufani katika shauri la Depson Balyagati dhidi ya Veronica J. Kibwana, Rufaa ya Madai Na. 21 of 2021 [2023] TZCA 17772 (23 Octoba 2023 ) , ambapo Mahakama ilielekeza kuwa wakati wa kutembelea eneo la mgogoro ni muhimu kuzingatia yafuatayo;

  1. Kuhakikisha kuwa wahusika wote wa shauri, mashahidi wao na mawakili wao, kama wapo, wanahudhuria ukaguzi wa eneo la mgogoro;

  2. Kuwapa wahusika na mashahidi wao fursa ya kutoa ushahidi katika eneo la mgogoro;

  3. Kuruhusu mashahidi kudodoswa (cross-examination) na kila upande au wakili wake dhidi ya mashahidi wa upande mwingine;

  4. Kuandika mwenendo wote wa shughuli zinazofanyika katika eneo la mgogoro; na Kurasa. 15

  5. Kuandika uchunguzi, maoni, tathmini au hitimisho lolote la Baraza, ikiwemo kuchora ramani ya eneo (sketch plan) pale inapohitajika. Kwa kuwa kasoro iliyosababisha kufanikiwa kwa rufani hii kumetokana na mwenendo wa Baraza, si kosa la upande wowote , ninaamru kila upande ubebe gharama zake. Imetolewa katika AKAMA KUU YA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA MASJALA NDOGO KIGOMA INAYOKETI KIGOMA tarehe 2 Juni 2026. A. K RWIZILE JAJI Kurasa. 16

Discussion