Mbezi Mgaaza Mkomwa vs Salum Said Salum and Others (Shauri la Rufaa la Ardhi Na. 18337 la Mwaka 2025) [2025] TZHC 8675 (19 Disemba 2025)
Judgment
KATIKA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA MAHAKAMA KUU YA TANZANIA DIVISHENI YA ARDHI DAR ES SALAAM SHAURI LA RUFAA LA ARDHI NA. 18337 LA MWAKA 2025 (Linatokana na maamuzi ya Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya ya Ilala kwenye Shauri la Maombi Na. 21 la mwaka 2025) MBEZI MGAZA MKOMWA (Msimamizi wa Mirathi ya Marehemu Shem Mohamed Mwinga na Inshaala Mohamed Mwiga) ................. MRUFANI DHIDI YA SALUM SAID SALUM (Msimamizi wa Mirathi ya Marehemu Athumani Mwiga) .................................................... MJIBU RUFAA WA KWANZA BI UBWA SAID SELEMANI ........................... MJIBU RUFAA WA PILI MUNDHIR MOHAMED MBARUK .................. MJIBU RUFAA WA TATU SUHAIFA MOHAMED MBARUK .................... MJIBU RUFAA WA NNE MBARUK MOHAMED MBARUK .................. MJIBU RUFAA WA TANO MUDRIK MOHAMED MBARUK .................... MJIBU RUFAA WA SITA SALWA MOHAMED MBARUK ..................... MJIBU RUFAA WA SABA SAMAH MOHAMED MBARUK .................... MJIBU RUFAA WA NANE PHILLIP JEREMIA MATEMU ........................ MJIBU RUFAA WA TISA HUKUMU Amri ya mwisho: 31/10/2025 Hukumu: 15/12/2025 MANGO, J Mrufani alifungua shauri la maombi Na. 21 la mwaka 2025 mbele ya baraza la ardhi na nyumba la wilaya ya Ilala akidai umiliki wa ardhi iliyosajiliwa kama 1
kiwanja Na. 25 Kitalu J Ilala Dar es salaam. Mjibu rufaa Na. 9 Phillip Jeremia Materu kupitia wakili wake, Goodluck Rweyemamu Kagande alileta pingamizi la awali kwamba shauri husika limepitwa na wakati na kwamba, shauri halikuwa sawa barazani kwa kushindwa kuunganisha wadaawa muhimu na baadhi ya wadaawa kuunganishwa kwa makosa. Baraza liliona pingamizi la kwamba shauri limepitwa na muda linamashiko na kulitupilia mbali shauri lililofunguliwa na mrufani kwa gharama. Mrufani hakuridhika na maamuzi hayo, akakata rufaa kwenye Mahakama hii akiwa na sababu zifuatazo:-
- Baraza la Wilaya la Ardhi na Nyumba la Wilaya ya Ilala lilikosea kisheria na kimantiki kwa kutamka kwamba mgogoro kati yangu na Wadaiwa upo nje ya muda bila kuzingatia kwamba tangu hati Na. 82018 ya Mdaiwa wa 9, Philip Jeremia Matemu ilipofutwa na serikali mnamo tarehe 05/08/2013 mpaka nilipofungua Maombi Na. 21 /2025 katika baraza la ardhi na Nyumba la Wilaya ya Ilala bado haijapita miaka kumi na mbili(12)
- Baraza la Wilaya la Ardhi na Nyumba la Wilaya ya Ilala lilikosea kisheria na kimantiki kwa kukubali na kusikiliza pingamizi la mjibu maombi akidai mgogoro kati yangu na wadaiwa upo nje ya muda bila kuzingatia kwamba tangu nilipoteuliwa kuwa msimamizi wa mrathi kupitia shauri la mirathi Na. 10/2019 na 1960/2023 na kuanza zoezi la kukusanya mali za marehemu bado sijafikisha miaka kumi na mbili(12)
- Baraza la Wilaya la Ardhi na Nyumba la Wilaya ya Ilala lilikosea kisheria na kimantiki kwa kukubali na kusikiliza pingamizi lililoibuliwa na mjibu maombi Na. 9 Phillip Jeremia Matemu akidai mgogoro huu uko nje ya muda bila kuzingatia kwamba nyaraka alizoingiza kwenye pingamizi 2
hati Na. 82018 ya kiwanja Na 25 Kitalu J kilichopo Ilala Mtaa wa Utete/ Nzasa ilifutwa na serikali tangu tarehe 05/08/2013 kwa barua yenye Kumbukumbu Na. AR/ ILA/ 874/RW 4. Baraza la Wilaya la Ardhi na Nyumba la Wilaya ya Ilala lilikosea kisheria na kimantiki kwa kukubali na kusikiliza pingamizi lililoibuliwa na mjibu maombi Na. 9 Phillip Jeremia Matemu huku akidai mgogoro kati yangu na wadaiwa uko nje ya muda bila kuzingatia kwamba nyaraka alizoingizwa na Mdaiwa wa 9 zilikwisha futwa na Serikali hazitambuliwi kisheria na huo ni wizi 5. Baraza la Wilaya la Ardhi na Nyumba la Wilaya ya Ilala lilikosea kisheria na kimantiki kwa kukubali na kusikiliza pingamizi lililoibuliwa na mjibu maombi Na. 9 Phillip Jeremia Matemu akidai mgogoro kati yangu na wadaiwa uko nje ya muda na kwamba sikuwaunganisha kwenye shauri Msajili wa hati, Kamishna wa Ardhi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali bila kuzingatia wao walitimiza wajibu wao wa kufuta hati Na. 82018 mnamo tarehe 05/08/2013 kwa barua yenye Kumb. Na. AR/ILA/874/RW 6. Baraza la Wilaya la Ardhi na Nyumba la Wilaya ya Ilala lilikosea kisheria na kimantiki kwa kukubali na kusikiliza pingamizi lililoibuliwa na mjibu maombi Na. 9 Phillip Jeremia Matemu huku akidai mgogoro kati yangu na wadaiwa uko nje ya muda bila kuzingatia kwamba mimi kwa sasa ndiye msimamizi ninawajibika kutafuta mali za marehemu wangu na kuzikusanya 7. Baraza la Wilaya la Ardhi na Nyumba la Wilaya ya Ilala lilikosea kisheria na kimantiki kwa kukubali na kusikiliza pingamizi lililoibuliwa na mjibu 3
maombi Na. 9 Phillip Jeremia Matemu huku akidai mgogoro kati yangu na wadaiwa uko nje ya muda kwa vile alionesha upendeleo wa dhahiri dhidi ya mjibu maombi Na. 9. Shauri la rufaa liliendeshwa kwa njia ya maandishi, maelezo ya Mrufani yaliletwa Mahakani na Mrufani mwenyewe wakati Mjibu Rufaa Na. 9 aliwakilishwa na wakili msomi, Goodluck Rweyemamu Kagande. Kwenye maelezo yake , Mrufani ameeleza kwamba shauri mbele ya baraza halikuwa limepitwa na muda kwa sababu mgogoro juu ya ardhi inayobishaniwa umeanza rasmi mwaka 2019 na 2023 pale alipoteuliwa kuwa msimamizi wa Mirathi wa Shem Mohamed Mwiga na Inshallah Mohamed Mwiga ambao ndio walikuwa wamiliki wa eneo hilo. Wakili wa mjibu rufaa ameeleza kwamba shauri lilikuwa nje ya muda kwa kuwa limefunguliwa miaka 35 baada ya kifo cha Shem Mohamed Mwiga. Na kwamba wakati wa uhai wake, marehemu Shem Mohamed Mwiga aliuza ardhi husika kwa Mohamed Mbaruk Said. Wakili wa mjibu rufaa wa tisa ameeleza zaidi kwamba kiwanja husika si sehemu ya mirathi ya marehemu Shem Mohamed Mwiga wala Inshallah Mohamed Mwiga kwakuwa kiliuzwa na Shem Mohamed Mwiga wakati wa uhai wake. Ameongeza pia mirathi ya Inshallah Mohamed Mwiga ilishafunguliwa na watoto wake na kufungwa hivyo mirathi inayodaiwa kufunguliwa na mrufani ni batili. Nimezingatia hati ya madai iliyoanzisha shauri mbele ya Baraza la Ardhi na nyumba la Wilaya ya Ilala, maamuzi ya baraza kuhusu pingamizi lililoibuliwa na Mjibu rufaa namba 9, na maelezo yaliyoletwa na pande zote mbili kwa maandishi. 4
Ni jambo linalofahamika wazi kwamba pingamizi la awali linapaswa kuwa limejengwa kwenye misingi ya sheria kama ilivyoelekezwa kwenye kesi ya Mukisa Biscuit Manufacturing Co. LTD dhidi ya West End Distributors LTD (1969) EA 696 na nyinginezo nyingi. Pingamizi la awali linalohusu ukomo wa kufungua shauri kudai umiliki wa ardhi inayobishaniwa linamchanganyiko wa masuala ya kiushahidi na kisheria. Nimeona hivyo kwa kuwa haibishaniwi kwamba ardhi husika iliwahi kumilikiwa na Marehemu Shem Mohamed Mwiga na Inshallah Mohamed Mwiga ambao mirathi yao inadaiwa kusimamiwa na Mrufani. Kwa upande wa Mrufani anadai kuwa amepata kujua kuhusu mgogoro juu ya umiliki wa kiwanja hicho mnamo mwaka 2019 hadi 2023 wakati alipokuwa anakusanya mali za marehemu hao wawili. Kwa upande wa mdaiwa wa tisa anadai kwanza, kiwanja husika kiliuzwa na marehemu Shem Mohamed Mwiga wakati wa uhai wake. Pili kwamba mirathi ya Inshallah Mohamed Mwiga ilishafunguliwa na kufungwa na watoto wake. Tatu, kwamba kesi za mirathi zilizofunguliwa na mrufani ni batili. Kimsingi masuala yote yaliyoibuliwa na wakili wa mjibu rufaa wa tisa yanapaswa kuthibitishwa kwa ushahidi ambao kwa bahati mbaya hauwezi kuletwa sawasawa mbele ya Baraza kabla ya usikilizwaji wa shauri husika. Taratibu zinataka pale Mahakama inapoketi kuamua pingamizi la awali, isiruhusu ushahidi wa aina yoyote. Baraza lilipoketi kuamua pingamizi la awali lilizingatia kuchelewa kwa kufunguliwa kwa mirathi bila kuangalia hati ya madai iliyo mbele yake inaonesha chanzo cha mgogoro kimeanza lini. Nakubaliana kwamba kipengee cha 22 kwenye jedwali la tisa la sheria ya ukomo wa muda, Sura ya 89 kama ilivyo kwenye juzuu za mwaka 2023 na 5
kufungu cha 9 sheria hiyo, vinasema madai yanayohusu ardhi iliyoachwa na marehemu yanapaswa kupelekwa mahakamani ndani ya miaka 12 tangu kifo cha marehemu. Hata hivyo ni ukweli usiopingika kwamba mdaawa hawezi kufungua shauri mahakamani kama hakuna mgogoro wowote. Hivyo, kifungu kidogo cha kwanza na cha pili cha kifungu Na. 9 cha sheria ya ukomo wa muda vinapaswa kusomwa na kutafsiri pamoja. Vifungu hivyo vinasomeka kama ifuatavyo:-
- Where a person institutes a suit to recover land of a deceased person, whether under a wi l or intestacy and the deceased person was, on the date of his death, in possession of the land and was the last person entitled to the land to be in possession of the land, the right of action shall be deemed to have accrued on the date of death . (Emphasis added)
- Where the person who institutes a suit to recover land, or some person through whom he claims, has been in possession of and has, while entitled to the land, been dispossessed or has discontinued his possession, the right of action sha l be deemed to have accrued on the date of the dispossession or discontinuance. Wakati kifungu 9(1) kinaonesha wazi kwamba kuhesabika kwa muda wa ukomo wa kufungua madai yanayohusu ardhi iliyoachwa na marehemu unachukuliwa kuanza kuhesabika pale marehemu anapokuwa amekufa, Kifungu 9(2) hakijafumbia macho mazingira ambapo wakati wa kifo cha marehemu hakukuwa na mgogoro wowote unaopaswa kufikishwa mahakamani. Kwa mantiki hiyo, naona kama suala kwamba shauri mbele ya baraza limepitwa na muda au la lilipaswa kuwa sahemu ya masuala yatakayofanyiwa maamuzi na Baraza baada ya kuwasililiza wadaawa ili kupata ushahidi kuhusu lini hasa mgogoro ulianza. Baada ya usikilizwaji, 6
Baraza litakuwa kwenye nafasi nzuri zaidi ya kuangalia masuala mengine kama vile madai ya kuuzwa kwa kiwanja husika na marehemu Shem Mohamed Mwiga kabla ya kifo chake. Suala la kutounganishwa kwa wadaawa muhimu na kuunganishwa kwa wadaawa wengine kimakosa halijafanyiwa maamuzi na Baraza, hivyo Mahakama hii haiwezi kuyatolea maamuzi yoyote. Kwasababu zilizoelezwa kwenye maamuzi haya naona kwamba rufaa hii inamashiko na inakubaliwa bila gharama. Amri za Baraza kulifuta shauri na gharama zinaondolewa. Shauri linarudishwa Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya ya Ilala kwa ajili ya kuendelea na usikilizwaji. Imetolewa Dar es salaam leo tarehe 19 Desemba 2025 Z.D.MANGO JAJI 7